I made this widget at MyFlashFetish.com.

DarLeo

Usikubali kupitwa na Darleo kila siku jioni kwa Habari na matukio ya leo leo. Gazeti pekee la kila siku jioni. Sasa limesheheni habari moto moto kutoka mtaani kwako.

Friday, October 1, 2010

Trafiki watakiwa kuongeza usalama Zakhem

Na Mwandishi Wetu, jijini

ASKARI wa Usalama Barabani wameombwa kuweka ulinzi mkali katika eneo la kituo cha Zakhem, Mbagala ili kupunguza kero ya foleni inayosababishwa na madereva kupakia abiria wakiwa wamesimama barabarani.

Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya abiria wamedai kuwa kutokana na kuwepo kwa kero hiyo, kumekuwa na foleni kubwa katika eneo hilo.

Wamedai kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wakishindwa kufuata sheria na kusimama barabarani bila ya kujali usalama wa abiria.

"Eneo hilo hivi sasa limekuwa kero hasa nyakati za jioni na hiyo yote inatokana na madereva kuegesha magari yao barabarani huku wakipakia abiria na kusababisha gari la nyuma kushindwa kuendelea na safari, " amedai mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Daud Hosea.

Amedai kuwa ili kuondokana na kero hiyo ni bora askari wakaongeza juhudi za kuweka ulinzi ili kuwabaini madereva hao wasiopenda kufuata sheria za usalama barabarani.

Naye Emmanuel Joakimu, mkazi wa Mbagala Kibonde Maji amedai kuwa kero hiyo pia imechangia kuwepo kwa baadhi ya madereva kukatisha ruti na kusababisha kuwepo kwa usafiri mgumu.

"Madereva wengine wanaamua kukatisha ruti kwani kitendo cha kufika hadi Mbagala Rangi Tatu inaweza ikamchukua saa moja ambapo umbali wake ni mdogo sana, " amedai mkazi huyo.

Mwandishi wa gazeti hili pia alishuhudia kuwepo kwa msongamano wa magari katika kituo hicho ingawa pia hali hiyo inachangiwa na ufinyu wa kituo cha Mbagala Mwisho na magari kushindwa kupishana.

Madereva wapongeza polisi kuwapiga wenzao makofi

Na Stella Aron, Mombasa

BAADHI ya madereva wamewapongeza Askari wa Usalama Barabarani na wale wa kutuliza ghasia (FFU) kwa kuwaadhibu kwa kuwapiga makofi wenzao wanaokiuka sheria za barabarani

Madereva hao wanaoanza safari zao katikati ya jiji kuelekea Gongo la Mboto, wamepongeza adhabu hiyo inayofanywa papo kwa papo na askari hao waliopo kituo cha Mombasa.

Wakizungumza na Dar Leo kwa nyakati tofauti, baadhi ya madereva hao wamedai kuwa kutokana na kuanzishwa kwa adhabu hiyo, kumesaidia kupunguza kuwepo kwa madereva wanaopita pembeni wakati mwingine hata misongamano.

"Tunawapongeza askari hao kutokana na kuweza kukabiliana na madereva hao ambapo hivi sasa kero hiyo imepungua, " amedai dereva mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Omary, anayeendesha gari aina ya DCM kutoka Gongo la Mboto kwenda Kariakoo.

Kassim Swalehe, anayeendesha gari litokalo Gongo la Mboto kwenda Ubungo, hali kadhalika amepongeza adhabu hiyo inayotolewa na polisi.

"Kweli tunawashukuru hawa askari kwani ilikuwa kero kubwa sana ambayo ilikuwa ikisababishwa na sisi wenyewe, hata hivyo tunaomba tabia ya kuwachapa vibao madereva wasiopenda kufuata sheria za barabarani iendelee na hata kwa maeneo mengine, " amedai dereva huyo.

Hivi karibuni Kamanda wa Usalama Barabarani nchini , Mohamed Mpinga alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa foleni kwenye maeneo ya nje ya mji, vikosi mbalimbali vya usalama vimekuwa vikisaidia ili kupunguza kero hiyo.

Thursday, September 30, 2010

Niliyoyaona njiani nikiwa kwenye daladala, Big Up bloggers wote. . .

 Upanga Aga khani, Polisi akiafungua namba za gari iliyotanua na kupita kwenye service road, Big Up Polisi...
 Nilipokuwa Magomeni kwenye mataa, mchana jua kali sana ilibidi abiria kwenye basi letu kununua mataulo kukausha jasho. . . Duh machinga wanasevu - Big Up Machinga...
 Vituo vyetu vimetimia, Mikocheni B hapo jamaa anauza mahindi ya kuchoma, kwa tuliovusha lanchi tunaponea hapo Big Up Mchoma mahindi...
 Jamaa wanahama Upanga, maisha ya upanga bei juu bana, swali ni je wanahamia wapi? Big Up wahamishaji. . .
 Huko Upanga nako hakuna nafuu yoyote na uswahilini kwetu, cheki jinsi shida ya maji ilivyotawala bongo, sasa katoto haka sijui shule kanaenda saa ngapi, hivi hakuna maji digital? Big up kaka msaidie dogo sio kumtazama...
 Mabondeni mpo...? haya nafikiri unapajua hapa, bonde la mkwajuni hilo mvua ikija sijui itakuwaje...
 Mkwajuni hapo, mambo ya kupakia mzigo kwenye daladala. . .
 Afadhali mi niko kwenye Daladala, cheki mshikaji kakaa juu ya maji...sijui tani ngapi hizo...Big Up Uhai
 Duu. . .mpaka sasa hali ndo hii. . . sijui itakuwaje leo. kijana muuza maji akitafakari katikati ya barabara Magomeni mapipa. . .Big up Muuza maji...
 Jamaa wanataka tuache kupanda daladala tuendeshe Pikipiki. . . ila na jua hili sijui itakuwaje Big Up pikipiki
 Sasa trafik akipumzika kivulini Vijana siwangetoa msaada, maana Mwenge ni balaa, hahaaaa. . . Big Up Trafik
 Mbezi mwisho hiyo... kituo au soko. . .Big Up mikokoteni. . .
 Hapa ndio lango la Jiji maana wengi mtapitia hapa kwa sasa mkitoka zenu bara huko Kwi kwi kwi. . . Big Up Ubungo
 Hizi kampeni zitatutoa roho. . .jamaa sijui kafikishaje picha kule juu. . .Big up kampeni
Sawa! hii ni kwa wale mnaodai ni shida kupanda daladala, cheki Kenya sasa hayo ndo mambo yalivyo upvountry Big up Rover...

Friday, September 17, 2010

Mzungu ndani ya daladala

Na Selma Steenhuisen na Athman Hamza.


"Nikiwa mmoja kati ya wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam tusio na usafiri wa binafsi, nimelazimika kutegemea daladala.
Muda wa msongamano barabarani siku zote hunipa hisia maalum. Kadri unavyokuwa na haraka ya kuwahi sehemu, ndivyo daladala linavyoenda taratibu na kadri unavyoomba upate siti upumzishe miguu iliyochoka, ndivyo unavyojiongezea uwezekano wa kupinda mgongo mpaka mwisho wa safari yako.
Ni vigumu kwa siku kupita ndani ya daladala bila kupata kitu cha kukumbuka," anasema  Selma Steenhuisen ambaye ni raia wa Uholanzi.

Dada huyu wa Kiholanzi ambaye amekuwa akija Tanzania kila msimu wa kiangazi tangu mwaka 2000, ndivyo alivyoanza  kutoa uzoefu wake wa usafiri wa daladala wakati akizungumza na gazeti hili.

Katika safu hii tutakuwa tunawaletea wasomaji wetu uzoefu wa wazungu na usafiri wa daladala, kitu ambacho kimekuwa kikiwafanya kupenda na kutosahau mikikimikiki ya usafiri huo katika maisha yao yote.


Safari ya Mtoni Mtongani-Kawe

Mwanadada huyo ambaye amekwenda hewani kisawa sawa, ananza simulizi zake kwa kusema "wakati napanda daladala konda alikuwa tayari katikati ya maonyesho ya kuchekesha kwani gari zima walikuwa wakiangua vicheko kutokana na uhodari wa konda huyo katika kufanya vibweka.

Kama mchekeshaji haswa akiwa jukwaani, abiria tukiwa kama watazamaji, abiria wakaanza kumtania kwamba hana ubavu wa kuongea na mzungu (yaani mimi) na hapo ndipo ukawa mwisho wa jeuri yake, mie nikakaa kimya nikisubiri kibweka cha mchekeshaji huyo hodari.

Haikuchukua muda ili aanze kukusanya nauli kutoka kwetu, alianza kibweka kingine kwa kusema,  "najua jinsi ya kuongea na mzungu, mimi siwaogopi hawa wazungu ni kama wanyama tu, hivyo siwezi kuwaogopa.

Unajua wanapotaka kusema 'nani' wanasemaje?, "whooff" (kama mbwa). whooof, whoof (yani kama mbwa tu)".

Kutokana na vibweka hivyo vya konda, abiria wa basi zima waliangua kicheko na kufanya nami pia nishindwe kujizuia. Wakati naangua kicheko, abiria nao wakazidi kucheka baada ya kugundua nami nimeelewa.

Usipitwe na makala haya. Wiki ijayo tutakuletea safari ya njia nyingine. Kumbuka ni kila Alhamisi.

Njemba yataka kufanya mapenzi ndani ya daladala *lililewa chakari*

Na Godfrey Ismaely, jijini

MKAZI mmoja wa jijini ambaye alikuwa amepanda daladala lenye namba za usajili T169 ASY aina ya DCM ambalo lilikuwa linafanya safari zake kati ya Mbagala na Buguruni, jana alisababisha tafrani katika daladala hilo baada ya kuanza kuwapiga busu abiria wasichana.

Tafrani hiyo ilijitokeza saa 11:30 jioni ambapo daladala hilo lilikuwa likiendelea na safari zake za kawaida ndipo njemba huyo ambaye alikuwa amelewa chakari,  alianza kuangaza macho kwa kila abiria, akiwa amesimama.

Ghafla katika viti vya nyuma aliwaona kinadada watatu ambao walikuwa ni ndugu, bila kujali kuwa kitendo hicho ni aibu, aliwasogelea na kuanza kusema sema hovyo.

"Toto's mbona kimya au mfungo wa Ramadhan umewanyima raha? kama ndio hivyo mimi subiri niwape raha" bila kujali alianza kuwapiga busu mmoja baada ya mwingine," ililalamika njemba hiyo.

Aliendelea kulalamika, "mimi kama ni fedha nimewekeza kweli katika mfungo wote wa Ramadhan, so what i need it's only toto's who will spend all money which had save for holy Ramadhan month so still smile, ok. Kama nimelewa nimelewa kwa sababu leo ninazo fedha, unaziona hizi noti za sh. 10,000, zipo saba mimi si tajiri".

Aidha baada ya wafanyakazi wa daladala hilo kushuhudia hali hiyo, waliwataka kinadada hao kutulia bila kubishana na njemba hiyo, lakini bila ya kujali aliendela na vituko vyake hivyo.

"Abiria wangu, ninawaombeni mtulie, hivi ni baadhi tu ya vituko vinavyotokea katika kazi zetu hizi za daladala hivyo huyo jamaa msibishane naye na atashuka muda si mrefu kwani bado kidogo tufike mwisho wa kituo," alitahadharisha kondakta wa daladala hilo aliyejitambulisha kwa jina la Ramadhan Mohamed.

Hata hivyo, baada ya njemba huyo kuona kuwa abiria wote wameanza kumjadili ili kutafuta namna ya kumdhibiti kutokana na kuwadhalilisha wasichana hao,  alipofika katika kituo cha TAZARA, alishuka huku akiwa anapiga kelele, "mkojo....unanibana au nikojoe humu ndani....".

Wednesday, September 15, 2010

Barabarani leo

Serilkali yaombwa kuingilia kati ajira za madereva

Na Godfrey Ismaely, Jijini

SERIKALI imeombwa kuingilia kitendo cha baadhi ya wamiliki wa daladala kuwabadilisha wafanyakazi wao kila siku hivyo kuondoa umakini na kuwanyima haki walengwa.

Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na wafanyakazi wa daladala zinazofanya safari zake kati ya Mnazi Mmoja na Tabata Segerea wakati wakizungumza na gazeti hili katika kituo cha Mnazi Mmoja kuhusu kutokuwa na mahusiano ya kutosha na matajiri wao.

"Sisi hapa tunabadilishwa kila siku kama nguo bwana, aheri serikali iweke mkazo kuhusu muda gani ambao tunatakiwa kudumu katika daladala moja kwani hata ile heshima inakuwa hamna tena licha ya kutunyima haki na kutufanya tukose umakini katika hii kazi," amesema dereva mmoja wa daladala aina ya DCM aliyejitambulisha kwa jina la Efferi Mohamed.

Ameongeza kuwa tangu aanze kufanya kazi ya udereva miaka miwili iliyopita amekuwa akiamishwa daladala baada ya daladala kwa madai kuwa hamna mtu mwenye hati miliki ya kukaa siku zote kuendesha daladala.

"Hata sisi hatupendi kuendesha daladala hizi ila tunalazimika kwa sababu hatuna jinsi, lakini inapofikia hatua mmiliki anakuambia kuwa mwenye "mandete" ya kutoa amri yeyote juu ya daladala husika na kukufukuza wakati ujajipanga huu ni unyanyasaji au unaambiwa una hati miliki hilo ndio suala gani tena," ameendela kusisitiza  dereva huyo Mohamed.

Naye mfanyakazi mwingine wa daladala hizo aliyejitambulisha kwa jina moja la Lema amesema kuwa licha ya kuelezwa kila siku kuwa kuna mchakato wa kupatiwa mikataba ya ajira katika daladala zoezi hilo linaweza lisifanikiwe vyema.

"Kwanini niseme hivyo ni kwa sababu uwajibikaji hauonekani hivyo tunahitaji kwanza serikali ilitupie macho suala la kuhimiza mahusinao mazuri kati yetu na wamiliki wote wa daladala la si hivyo tutakuwa tunawapigia mbuzi gitaa," amesema Lema.

Tuesday, September 14, 2010

Baadhi ya wafanya biashara wakisubiri Daladala katika kituo cha mabasi cha Rozana Buguruni. Gharama nafuu za kupakia bidhaa katika daladala kunasaidia kupunguza mfumuko wa bei za bidhaa za mashambani na viwandani.

Saturday, September 11, 2010

Kituo cha Daladala

Kituo cha Kwenda Tandika kilichopo shule ya uhuru, Kariakoo. Licha ya ubovu wa kituo hicho hulalamikiwa kwa muda mrefu sasa hali imeendelea kuwa hivyo kama ilivyokutwa hali ambayo husababisha foleni hususani nyakati za jioni.(Picha na Mpiga Picha wetu)

 


Thursday, September 9, 2010

Sababu za daladala kukatiza ruti zatajwa


Na Athman Hamza.

Kiwango cha nauli katika baadhi ya njia ndio sababu kubwa ya daladala kukatiza ruti Darleo limeelezwa. viango hivyo vidogo ukilinganisha na umbali wa safari huwalazimu madereva kuishia njiani au kuanza kupakia katikati ya ruti hususani maeneo ambayo abiria wakipanda hawashukii njiani.

Hayo yameelezwa na baadhi ya madereva wa daladala zifanyazo kazi yake kati ya Kawe na Buguruni wakati wakiongea na gazeti hili kuhusiana na sababu ya wao kuacha kupakia abiria mwanzo wa safari au kutangaza wanaishia njiani wakati wanaenda ampaka mwisho wa ruti.

Made reva hao wamesema kiwango cha nauli kikiwa kidogo na abiria kutaka kupanda mwanzo mpaka mwisho wa ruti inakuwa shida kupata hesabu ya siku hivyo kupelekea kuweka ajira zao hatiani.

"Ukiangalia ruti ya kawe buguruni na tabi ya abiria wa ruti hii utaona sababu ya sisi kusema tunaishia magomeni kwani abiria wakipanda hawashuki mpaka mwisho wa ruti" alisikikika dereva aliejitambulisha kwa jina la moja la Onesmo

Nae dereva Mrisho kasinde amesema bei ya nauli ya Buguruni Kawe na Buguruni- Msasani ni moja ya sababu inayofanya madereva kukatisha ruti na kuomba bei ya njia hizo kuangaliwa upya ili kuondoa tatizo hilo.
Abiria wa waendao Gongo la Mboto wakigombea kuindgia ndani ya daladala kutokana na adha ya usafiri nyakati za jioni kama walivyokutwa na mpiga picha wetu jana katika kituo cha basi cha Shule ya Uhuru.