I made this widget at MyFlashFetish.com.

DarLeo

Usikubali kupitwa na Darleo kila siku jioni kwa Habari na matukio ya leo leo. Gazeti pekee la kila siku jioni. Sasa limesheheni habari moto moto kutoka mtaani kwako.

Tutagombania Daladala mpaka lini?


Na Athman Hamza.

Kwa mgeni wa jiji la Dar es salaam hususani wale watokao nje ya nchi ukiwauliza ni kipi wanachokikumbuka pindi wanaposikia neno Dar es salaam, wengi wao watakwambia daladala, neno lililojizolea umaarufu mkubwa kutokana na shida ya usafiri jijini. Lakini watu hao hao ukiwauliza kipi wasichopenda katika daladala watakwambia ni utaratibu wa upandaji daladala ambapo kwa watu waliostaarabika na wanaoheshimu na kutambua haki zao ni kitendo kigeni sana kwao.

Hali huwa hivyo hivyo ukiwauliza wakazi wengi wa jiji hili kwamba ni kitu gani wasichokipenda kutoka katika daladala. Wengi wao wamekuwa wakilalamika kwamba kutokuwepo kwa utaratibu wa upandaji daladala ni moja ya kero kubwa zinazowakabili watumiaji wa daladala hali ambayo inasababisha wenye nguvu na uwezo wa kugombania kuwa na uwezo wa kuchukua haki ya waliowahi.

Ukienda katika nchi za wenzetu au zile zilizoendelea katika suala la kutambua na kuheshimu haki ya kila mmoja huwezi kuta tatizo la kugombania kuingia katika mabasi ya abiria kwani wakwanza kufika kituoni ndio atakuwa wakwanza kupanda gari. Ukichukulia mfano wa majirani na ndugu zetu wa kenya unaweza ukaona kwa jinsi gani wenzetu wanavyotambua na kuheshimu haki ya kila mmoja kwani hata ukienda katika kituo cha matatu saa mbili usiku utakuta abiria wamepanga foleni kusubiria magari.

Kukosekana kwa utaratibu wa kupanda daladala katika jiji la Dar es salam ni kipimo tosha cha kuonyesha jinsi gani wakazi wa jiji hili wasivyo na mazoea ya kutambua na kudai haki zao na pia kutokuwa na mazoea ya kutambua na kuheshimu haki za wengine. Kama utaratibu wa kupanga foleni utaanzishwa jijini si tu utaondoa kero wakati wa upandaji daladala bali pia utasaidia katika kampeni za rushwa kwani watu wakielewa umuhimu wa kutambua na kuheshimu haki ya alietangulia kufika
kituoni itasaidia pia kutatua tatizo la watu wanaotoa rushwa ili wawahi kuhudumiwa katika mahospitali, mashuleni na sehemu nyingine za huduma za kijamii. Pia utaratibu huo utasaidia makundi ya wasiojiweza kama wagonjwa, watoto, walemavu na wazee kwani imekuwa shida sana kwao kupata usafiri nyakati za asubuhi na jioni.

Kama kupanga foleni kunawezekana katika mabenki na kukata tiketi za kuingia uwanja wa taifa inashindikana vipi katika vituo vya daladala?