Na Selma Steenhuisen na Athman Hamza.
"Nikiwa mmoja kati ya wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam tusio na usafiri wa binafsi, nimelazimika kutegemea daladala.
Muda wa msongamano barabarani siku zote hunipa hisia maalum. Kadri unavyokuwa na haraka ya kuwahi sehemu, ndivyo daladala linavyoenda taratibu na kadri unavyoomba upate siti upumzishe miguu iliyochoka, ndivyo unavyojiongezea uwezekano wa kupinda mgongo mpaka mwisho wa safari yako.
Ni vigumu kwa siku kupita ndani ya daladala bila kupata kitu cha kukumbuka," anasema Selma Steenhuisen ambaye ni raia wa Uholanzi.
Dada huyu wa Kiholanzi ambaye amekuwa akija Tanzania kila msimu wa kiangazi tangu mwaka 2000, ndivyo alivyoanza kutoa uzoefu wake wa usafiri wa daladala wakati akizungumza na gazeti hili.
Katika safu hii tutakuwa tunawaletea wasomaji wetu uzoefu wa wazungu na usafiri wa daladala, kitu ambacho kimekuwa kikiwafanya kupenda na kutosahau mikikimikiki ya usafiri huo katika maisha yao yote.
Safari ya Mtoni Mtongani-Kawe
Mwanadada huyo ambaye amekwenda hewani kisawa sawa, ananza simulizi zake kwa kusema "wakati napanda daladala konda alikuwa tayari katikati ya maonyesho ya kuchekesha kwani gari zima walikuwa wakiangua vicheko kutokana na uhodari wa konda huyo katika kufanya vibweka.
Kama mchekeshaji haswa akiwa jukwaani, abiria tukiwa kama watazamaji, abiria wakaanza kumtania kwamba hana ubavu wa kuongea na mzungu (yaani mimi) na hapo ndipo ukawa mwisho wa jeuri yake, mie nikakaa kimya nikisubiri kibweka cha mchekeshaji huyo hodari.
Haikuchukua muda ili aanze kukusanya nauli kutoka kwetu, alianza kibweka kingine kwa kusema, "najua jinsi ya kuongea na mzungu, mimi siwaogopi hawa wazungu ni kama wanyama tu, hivyo siwezi kuwaogopa.
Unajua wanapotaka kusema 'nani' wanasemaje?, "whooff" (kama mbwa). whooof, whoof (yani kama mbwa tu)".
Kutokana na vibweka hivyo vya konda, abiria wa basi zima waliangua kicheko na kufanya nami pia nishindwe kujizuia. Wakati naangua kicheko, abiria nao wakazidi kucheka baada ya kugundua nami nimeelewa.
Usipitwe na makala haya. Wiki ijayo tutakuletea safari ya njia nyingine. Kumbuka ni kila Alhamisi.
